Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tarehe 25 Aprili ni Siku ya Malaria Duniani, hatua zimepigwa kutokomeza ugonjwa huo

Tarehe 25 Aprili ni Siku ya Malaria Duniani, hatua zimepigwa kutokomeza ugonjwa huo

Jumapili ya tarehe 25 Aprili ni siku ya malaria duniani na siku hii inaadhimishwa zikiwa zimesalia siku 250 kutimiza changamoto iliyowekwa na Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa . Changamoto hiyo ni kwa nchi zote zenye matatizo ya malaria kuweza kufikia malengo ya kudhibiti ugonjwa huo ifikapo desemba 31 mwaka huu.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe wake maalumu wa kuadhimisha siku hiyo amesema miaka miwili iliyopita alitoa wito wa kuwepo na programmu za kukinga na kutibu malaria kwa wote ambao wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Amesema siku ya malaria mwaka huu inaleta faraja na kuridhika kwani katika kipindi cha muda mfupi dunia imepiga hatua kutoka kujitahidi kupambana na ugonjwa huo hadi hatua ya kufikia lengo la kutoa huduma ambayo inapatikana kwa urahisi kwa wote wanaoihitaji.