Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matatizo ya utapia mlo kwa watoto wadogo yamekithiri Somalia

Matatizo ya utapia mlo kwa watoto wadogo yamekithiri Somalia

Kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu ICRC imeonya kwamba utapa mlo kwa watoto wadogo Somalia unaongezeka kwa kiasi kikubwa.

Shirika hilo linasema hali ya kibinadamu bado ni mbaya nchini humo kutokana na mapigano yanayoendelea baina ya vikosi vya serikali na makundi ya wanamgambo na pia tatizo la ukame katikati mwa nchi hiyo. Msemaji wa ICRC Nicole Engelbrecht anasema visa vya utapia mlo uliokithiri vimeongezeka karibu mara mbili katika baadhi ya maeneo ya Somalia na hususani kusini na katikati mwa nchi hiyo.

Katika baadhi ya sehemu utapia mlo umepanda kwa asilimia 30, na mwezi wa pili mwaka huu visa vilikuwa 115 lakini mwezi huu wa Aprili vimefikia 350. ICRC kwa kushirikiana na serikali ya Somalia wanafuatilia kwa karibu hali hii na kuimarisha huduma za afya, lishe, huduma ya maji salama na uzalishaji wa mazao.