Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado kuna changamoto ya kupata kinga na matibabu ya HIV barani afrika

Bado kuna changamoto ya kupata kinga na matibabu ya HIV barani afrika

Afisa wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya ukimwi amesema licha ya hatua zilizopigwa kukabiliana na ukimwi Afrika bado kuna changamoto nyingi zinazowafanya watu kushindwa kupata kinga na matibabu yanayohitajika.

Afisa huyo ambaye ni mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na ukimwi UNAIDS Michel Sidibe, ameyasema hayo akiwa ziarani nchini Senegal. Amesema katika mwaka 2008 asilimia 45 ya wanawake wajawazito wanaoishi na virusi vya HIV barani Afrika walikuwa wakipata dawa za kurefusha maisha ili kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto tofauti na mwaka kabla ya hapo ambapo ilikuwa ni asilimia 35 tuu.

Amesema pamoja na hatua hiyo iliyopigwa kutokana na juhudi za serikali za Afrika, jumuiya za kijamii na vijana, bado kuna changamoto ,hasa upatikanaji wa dawa na matibabu unahitaji kuimarishwa kwani ukimwi umekuwa ndio chanzo cha vifo vingi vya watoto katika maeneo mengi ya Afrika. Mwaka 2008 karibu watoto 390,000 wa umri wa chini ya miaka 15 waliambukizwa virusi vya HIV.

Utokomezaji wa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ndio itakuwa ajenda kubwa kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika AU uliopangwa kufanyika Julai mwaka huu nchini Uganda.