Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shirika la fedha duniani IMF linasema uchumi wa dunia umeanza kuimarika

Shirika la fedha duniani IMF linasema uchumi wa dunia umeanza kuimarika

IMF inasema uchumi wa dunia umeanza kuimarika vyema kuliko ilivyotarajiwa ,lakini inasema kuimarika huko kunatofautiana katika sehemu mbalimbali duniani.

Katika taarifa ya karibuni ya mtazamo wa uchumi duniani IMF inasema katika nchi zilizoendelea kiuchumi Marekani imepiga hatua kubwa kuimarisha uchumi wake baada ya mdororo kuliko nchi za Ulaya na Japan. Na katika nchi zinazoendelea na kuchipuka kiuchumi Asia inaongoza kujiimarisha tena baada ya matatizo ya kiuchumi huku nchi nyingi zinazochipukia kiuchumi Ulaya na nchi za jumuiya ya Madola bado zinasuasua.

Uchina inatabiriwa kuwa uchumi wake utakuwa kwa asilimia 10 mwaka huu , huku India ukikuwa kwa kasi ya asilimia 8.8. Na nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara zimeelezwa kukabiliana vyema na mdororo wa uchumi na kuimarika kwa uchumi wake inasemekana kutakuwa imara zaidi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma za matatizo ya kiuchumi.