Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ametoa wito wa kuelekeza fedha zaidi katika kufadhili maendeleo kuliko kununua silaha

Ban ametoa wito wa kuelekeza fedha zaidi katika kufadhili maendeleo kuliko kununua silaha

Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa leo umejadili suala la upokonyaji silaha duniani. Katibu Mkuu Ban Ki-moon ametoa wito kwa dunia kubadili mtazamo wa matumizi yake ya ununuzi wa silaha na kutumia fedha hizo kwa ajili ya maendeleo.

Ban amesema dunia ina silaha nyingi sana na maendeleo hayafadhiliwi vya kutosha. Ban ameyasema hayo kwa wajumbe 192 wa mkutano huo ambao umeanza kujadili suala la upokonyaji silaha na usalama wa dunia, na wajibu wa Umoja wa Mataifa na changamoto kwa jumuiya ya kimataifa Amesema matumizi kwa ajili ya silaha duniani kote hivi sasa ni zaidi ya dola trilioni moja kwa mwaka na kila siku yanapanda.

Ban amesema sasa mambo yanayopewa kipaumbele inabidi yabadilike .Kwa kupunguza silaha tunaweza kutumia fedha hizo , kwa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kushughulikia matatizo ya chakula na kufikia malengo ya milenia ifikapo mwaka 2015 ikiwemo njaa na umasikini, vifo vya kina mama wajawazito na watoto, suala la elimu na huduma ya afya. Bwana Ban amegusia pia mambo yanayotia moyo kama mkutanio wa nyuklia wa wiki jana mjini Washington na mkataba uliosainiwa hivi karibuni baiana ya Urusi na Marekani wa kupunguza silaha za nyuklia akisisitiza kuwa huu ndio wakati wa kutekeleza azma hiyo."