Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Moshi wa Volkano nchini Iceland unaendelea kuzusha adha ya usafiri duniani

Moshi wa Volkano nchini Iceland unaendelea kuzusha adha ya usafiri duniani

Shirika la Umoja wa Mataifa la utalii UNWTO limetoa wito wa kuwepo na mshikamano baina ya nyanja ya usafiri na utalii na kutaka wasafiri watendewe haki.

Wito huo umefuatia kuendelea kuvurugika kwa ratiba za usafiri wa anga kutokana na moshi wa volkano Eyjafjalla nchini Iceland tangu April 14.

Moshi huo umesababisha viwanja vingi vya ndege kufungwa hususani barani Ulaya na shirika la usalama wa usafiri wa anga Ulaya linasema takribani ndege elfu 63 zimelazimika kufuta safari zake, na mamilioni ya watu nje na ndani ya Ulaya wameathirika na hatua hiyo.

UNWTO limezitaka pande zote binafsi na za umma kuwatendea haki wasafiri, kushirikiana ili kupunguza athari ya hatua hii na kuheshimu sheria za wasafiri. Nayo tume ya Ulaya imesisirtiza katika hali yoyote ile haki za msafiri ziko palepale ikiwepo ya kuchagua kurejeshewa fedha zake, kupewa malazi na chakula.