Mkuu wa UNESCO alaani mauaji ya mwandishi habari wa Japan
Mkurugenzi mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, leo amesema analaani mauaji ya mwandishi habari wa Japani na kujeruhiwa kwa mwingine mjini Bangkok, Thailand.
Hiroyuki Muramoto, mpiga picha wa shirika la Reuters alipigwa risasi kifuani na mtu mwenye silaha asiyejulikana wakati akiripoti maandamano ya kupinga serikali tarehe 10 Aprili na alitangazwa amefariki dunia mara tu alipofikishwa hospitali. Winnai Ditthajorn, mpiga picha wa kujitegemea aliyekuwa akilifanyia kazi shirika la habari la Australia ABC News, alilazwa hospitali baada ya kupigwa risasi kwenye mguu wake wa kushito, lakini hali yake sio mahututi.
Mkuu wa UNESCO amesema waandishi hao wawili walikuwa wanafanya kazi yao na matokeo yake ynazidi kuashiria hatari wanayokabiliana nayo waandishi habari jasiri kila siku, ili kwamba uhuru wa habari ambayo ni haki ya binadamu iweze kutimizwa. Bi Bokova ameutaka uongozi wa Thailand kuchunguza mauaji hayo ya Muramoto na kufanya kila juhudi kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi yao kwa usalama.