Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa UM Afghanistan anataka kuwe na juhudi mpya za kuwalinda raia

Mjumbe wa UM Afghanistan anataka kuwe na juhudi mpya za kuwalinda raia

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Staffan de Mistura ameelezea wasiwasi mkubwa alio nao juu ya vifo vya raia nchini humo.

 Siku ya Jumatatu raia wanne waliarifiwa kuuawa na wengine 18 kujeruhiwa katika wilaya ya Zhari jimbo la Kandahar wakati vikosi vya kimataifa vilipofyatua risasi kwenye basi.

Bwana de Mistura amesema ameshitushwa na tukio hilo na amezitaka pande zinazohusika katika mgogoro wa nchi hiyo kuchukua hatua za tahadhari ili kutofautisha baina ya raia na wapiganaji.

Mwakilishi huyo amesema hali hii hairidhishi na amesema juhudi zote lazima zichukuliwe ili kuhakikisha haitokei tena. Pia amesifu uamuzi wa jeshi la msaada wa kimataifa ISAF kuchunguza tukio hilo la Jumatatu.