Mwakilishi wa UM kuhusu malaria anasema kufikia lengo la kupunguza vifo zaidi ifikapo 2015 inawezekana
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu malaria, ugonjwa unaokadiriwa kuua watu milioni moja duniani kote kila kila mwaka amesema malaria itaacha kuwa muuaji mkubwa ifikapo mwaka 2015 endapo tuu dunia itaendeleza kasi iliyonayo ya kupambana na ugonjwa .
Mwakilishi huyo Ray Chambers amesema njia muafaka ya kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo hadi sifuri ifikapo 2015 ni kujitahidi kugawa vyandarua kwa watu wote wanaoishi nchi zinazosumbuliwa na malaria ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Kwa kufanya hivyo anatumai lengo litafikiwa na ikiwa wahisani wataendelea kufadhili kampeni ya mradi wa kutokomeza malaria. kampeni hiyo ya miaka miwili ina lengo la kuchagiza zaidi juhudi za kimataifa kuhakikisha vyandarua vya mbu vinapatikana kwa watu wote walio katika hatari na kupunguza vifo kwa silimia 50 ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2010.