Skip to main content

Kongamano la kimataifa la masuala ya uhalifu limeanza nchini Brazil

Kongamano la kimataifa la masuala ya uhalifu limeanza nchini Brazil

Wataalamu wa sheria za uhalifu na watunga sera wanakutana mjini Salvador, Brazil ili kuainisha umuhimu wa mfumo wa sheria katika maendeleo.

Kongamano hilo ni la 12 la Umoja wa Mataifa linalohusika na kuzuaia uhalifu na haki za kisheria.

Wataalamu na watunga sera hao wanashiriki kongamano hilo ili kusisitiza haja ya kuchukua hatua za kubadili mifumo ya sheria.

Kongamano hilo la uhalifu la Umoja wa Mataifa limekuwa likifanyika kila baada ya miaka mitano tangu mwaka 1955, na hili la mwaka huu litabainisha mifumo inayoibuka ya uhalifu na pia mifumo mipya ya uhalifu wa zamani kama uharamia ambao umekuwa tishio kwa jamii nyingi duniani.

Katika ujumbe maalumu alioutuma kwenye kongamano hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewataka washiriki kuwa hatua moja mbele ya wahalifu hususani unapoibuka uhalifu kama wa kutumia mtandao na ule wa mazingira.