Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upigaji kura kwenye uchaguzi wa Sudan waongezewa muda wa siku mbili

Upigaji kura kwenye uchaguzi wa Sudan waongezewa muda wa siku mbili

Uchaguzi mkuu nchini Sudan leo umeingia katika siku ya pili, huku taswira ya mambo ikiashiria kukiukwa kwa taratibu katika baadhi ya maeneo.

Ingawa siku ya kwanza ilionekana kuwa shwari mjini Khartoum katika baadhi ya maeneo vituo vya kupigia kura vilichelewa kufunguliwa na kwengineno havikufunguliwa kabisa. Na kutokana na kucheleweshwa kwa karatasi za kupigia kura katika baadhi ya vituo tume ya uchaguzi nchini humo imesema sasa muda wa kupiga kura umeongezwa kwa siku mbili zaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa taarifa akizitaka pande zote zinazohusika na uchaguzi nchini humo kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru bila ghasia wala vitisho. Sudan inapiga kura ya uchaguzi wa kidemokrasia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24. Watu milioni sita walijiandikisha kupiga kura ya uchaguzi huo wa Rais na wabunge.