UM kuimarisha ushirikiano na nchi zinazozungumza Kifaransa kupambana na ukimwi

1 Aprili 2010

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na mapambano dhidi ya ukimwi UNAIDS leo limeahidi kuimarisha ushirikiano na nchi 50 zinazozungumza Kifaransa katika kupambana na ugonjwa wa ukimwi.

Katika nchi hizo watu zaidi ya milioni nne wameathirika na ugonjwa huo. UNAIDS imechukua hatua hii wiki mbili baada ya kufanya vivyo hivyo kwa nchi zinazozungumza Kireno.

Mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Michel Sidibe katika kufunga kongamano la tano la ukimwi kwa nchi zinazozungumza Kifaransa mjini Casablanca Morocco, amesema anaona hatua hiyo ni ukurasa mpya wa ushirikiano. Nyingi ya nchi hizo zipo Afrika na nchi hizo zina watu wapatao milioni 800.

Bwana Sidibe amesema kwa kushirikiana na nchi hizo anaamini ndoto yake itatimia ya kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya HIV. UNAIDS inakadiria kuwa watu milioni 4.1 wanaishi na virusi vya HIV katika nchi zinazozungumza Kifaransa , na kwa mwaka 2008 pekee maambukizi mapya yalikuwa laki tatu na elfu arobaini.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter