Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 8 zimeahidiwa leo kwenye mkutano wa kuisaidia Haiti

Dola bilioni 8 zimeahidiwa leo kwenye mkutano wa kuisaidia Haiti

Nchi na mashirika mbalimbali wameahidi kutoa zaidi ya dola bilioni nane hii leo ili kuisaidia Haiti katika ujenzi mpya baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi.

Ahadi hizo zimetolewa saa chache tuu baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kufungua mkutano huo wa wahisani na kuwataka wajitolee kwa hali na mali. Katika hotuba yake ya ufunguzi asubuhi ya leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York bwana Ban aliwaomba wahisani kuchangia dola bilioni 11.5 katika kipindi cha miaka kumi ijayo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya Haiti.

Dola bilioni 3.9 kati ya msaada huo wa dola bilioni 11.5 zitaelekezwa katika miradi maalumu kupitia tume ya ujenzi mpya wa Haiti katika miezi 18 ijayo. Bwana Ban amesema ujenzi mpya lazima uende sambamba na misaada ya dharura na hivyo amewataka wahisani kutoa msaada zaidi kwa mahitaji ya dharura ambayo yanataka dola bilioni 1.4. Hadi sasa asilimia 50 ya fedha hizo zimepatikana