Skip to main content

Umoja wa Mataifa unachunguza mauaji ya raia yanayoendelea Congo RDC

Umoja wa Mataifa unachunguza mauaji ya raia yanayoendelea Congo RDC

Umoja wa Mataifa unaendelea na uchunguzi wake kufuatia kundi la Lords Resistance Army kufanya mauaji ya raia Kaskazini Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya congo Desemba mwaka 2009.

Zaidi ya watu 300 wamearifiwa kuuawa wakati wengine zaidi ya 200 inasemekana wametekwa na kundi hilo la waasi kutoka Uganda. Mapanga, shoka na miti vilitumika katika siku nne za mauaji kwenye kijiji cha Makombo ambako watoto takribani 80 wametoweka kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch.

Ripoti hiyo pia inaelezea jinsi wanaume walivyokuwa wakifungwa kamba kifuani na kutobolewa kwa vijiti nyuma ya viganja vyao na shingo. Umoja wa Mataifa umeshindwa kuthibitisha idadi kamili ya waliouawa hadi hapo uchunguzi wa mpango wa kulinda amani Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUC utakapokamilisha uchunguzi wake.

MONUC hivi sasa inatoa msaada kwa vikosi vya serikali katika operesheni dhidi ya waasi hao wa LRA, kundi lililoanzishwa nchini Uganda miaka ya 1980, ambalo viongozi wake wanatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kwa makosa ya uhalifu wa kivita.