Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waziri mkuu wa Iraq aukosoa UM kwa kutounga mkono kuhesabu upya kura

Waziri mkuu wa Iraq aukosoa UM kwa kutounga mkono kuhesabu upya kura

Waziri mkuu wa Iraq ameukosoa Umoja wa Mataifa kwa kutounga mkono madai yake ya kutaka kura za uchaguzi wa bunge wa Machi 7 zihesabiwe upya.

Kauli hiyo ni ya karibuni kabisa ya bwana Nouri ali-Maliki ya kupinga matokeo ya uchaguzi ambayo yalimuweka katika nafasi ya pili dhidi ya mpinzani wake anayeungwa mkono na Wasuni Ayad Allawi.

Katika kauli hiyo aliyoitoa jana Jumapili kwenye televisheni binafsi ya Al-Sumariya bwana Maliki ameukosoa vikali mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, uliosema uchaguzi ulikuwa wazi, huru na wa haki na hakukuwepo na udanganyifu.

Maliki anadai kulikuwepo na udanganyifu na wizi wa kura. Tume ya uchaguzi ya Iraq imekataa madai ya Maliki na kusema si ya lazima.