Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu limepitisha hatua za kuisaidia Congo DRC na Guinea

Baraza la haki za binadamu limepitisha hatua za kuisaidia Congo DRC na Guinea

Baraza la haki za binadamu leo limepitisha masuala saba muhimu ikiwemo njia za kuzisaidia kiufundi Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Guinea.

Masuala mengine yaliyopitishwa ni kuongeza muda wa mwakilishi maalumu wa hali ya haki za binadamu nchini Myanmar, pia masuala ya utesaji na ukatili, udhalilishaji na adhabu za kushusha utu wa mtu,haki za mtoto na mapambano dhidhi ya ukatili wa kimapenzi kwa watoto, ushirikiano wa kimataifa katika kupigania haki za binadamu, na ulinzi kwa waandishi wa habari hasa katika maeneo ya vita.

Katika suala la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baraza hilo limesema litasaidia katika mambo ya haki za binadamu kwa kuimarisha ushirikiano wa kiufundi na huduma za mawasiliano, pia limeiomba serikali ya congo kuendelea kuhakikisha ulinzi kwa waandishi wa habari.

Mbali ya hayo limeitaka pia serikali ya Congo kuhakikisha watetezi wa haki za binadamu wanalindwa na kupiga vita ukatili wa kimapenzi na kuwachukulia hatua wahusika pi wanaokiuka haki za binadamu, katika jeshi na polisi.

Na kwa upande wa Guinea baraza hilo limeomba jumuiya ya kimataifa kusaidia kuwepo uongozi wa mpito haraka iwezekanavyo, na kuwapa msaada unaostahili kama mchango wao wa kuhakikisha katiba inafuatwa, sheria zinazingatiwa na amani inarejea . Pia kuiunga mkono, serikali ya Guinea katika kuchagiza kuheshimu haki za binadamu.