Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kisiasa Jerusalem ni ya vuta ni kuvute baada ya mapigano

Hali ya kisiasa Jerusalem ni ya vuta ni kuvute baada ya mapigano

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema hali ya kisiasa mjini Jerusalem ni ya wasiwasi kufuatia mapigano baiana ya Israel na Wapalestina.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu mjini Jerusalem Philippe Lazzarin amesema siku zote kumekuwa na hofu lakini hali ya sasa imefurutu ada. Lazzarini ameyasema hayo katika mkutano leo na waandishi wa habari mjini Geneva kukiwa na matarajio ya kupiga kura kwenye baraza la haki za binadamu kuhusu hali ya Mashariki ya kati.

Amerejea msiammo wa Umoja wa Mataifa dhidi ya hatua ya Israel ya kutaka kujenga makazi mapya ya Walowezi Mashariki mwa Jerusalem eneo ambalo Wapalestina wanataka liwe mji mkuu wa taifa lao siku za usoni.

Afisa huyo amesema ukanda wa Gaza kuna mtafaruku mkubwa wa haki za binadamu na asilimia 80 ya watu wa eneo hilo wanaishi kwa kutegemea msaada kutoka mashirika mbalimbali. Makundi yasiyo ya kiserikali yanayoendesha shughuli zake nchini Israel yamekuwa yakikabiliwa na wakati mgumu , huku yakitiliwa mashaka na kukosolewa zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote.