Skip to main content

Mtaalamu wa haki za binadamu anataka vikosi vya UM vipelekwe Somalia

Mtaalamu wa haki za binadamu anataka vikosi vya UM vipelekwe Somalia

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufikiria tena wazo la kupeleka vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa Somalia

Akihutubia baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva leo Shamsul Bari amesema watu wa Somalia wameteseka kwa muda mrefu na njia zote za kuweza kumaliza miongo miwili ya vita lazima zidadisiwe na kutekelezwa kwa haraka.

Ameongeza kuwa raia wa Somalia wanataka kuona vita vinamalizika na wako tayari kuunga mkono upande wowote utakaoweza kuwaondolea jinamizi la machungu ya muda mrefu. Hata hivyo amesema si majeshi ya serikali ya mpito ya Somalia au wanamgambo wa Kiislam wa Al-Shabab ambao wako katika nafasi ya kuleta amani ya kudumu inayoliliwa na Wasomali.

Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa lazima ichukue jukumu la kukomesha kupotea kwa maisha ya watu, ukiukaji wa haki za binadamu na uvunjaji wa sheria za kimataifa unaoendelea Somalia.