Skip to main content

Kwa mara ya kwanza Jamhuri ya Korea imempa mkimbizi hadhi ya uraia

Kwa mara ya kwanza Jamhuri ya Korea imempa mkimbizi hadhi ya uraia

Kwa mara ya kwanza tangu kupitishwa mkataba wa wakimbizi 1951 Jamuhuri ya Korea imempa mkimbizi hadhi ya uraia. Mkumbizi huyo alikuwa anatambulika nchini humo na hatua ya leo ya kumpa uraia imepongezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kwa mujibu wa Melisa Fleming msemaji wa UNHCR hatua hii ni muhimu sana barani Asia ambako nchi chache tuu ndio zimetia saini mkataba wa wakimbizi wa mwaka 1951 na wachache zaidi wanatoa uraia kwa wakimbizi. Amesema UNHCR inaishukuru Jamuhuri ya Korea kwa uongozi wake unaoruhusu maingiliano ambayo ni moja ya mambo matatu muhimu ya suluhisho kwa wakimbizi, na jambo ambalo ni nadra kutendeka Asia.

Uraia, ameongeza Bi Fleming, ni mfumo mmoja muhimu wa kuruhusu maingiliano, na inaleta matumaini kwamba nchi nyingine za Asia zitafuata nyayo.

Jamuhuri ya Korea ilimtambua mkimbizi wa kwanza mwaka 2001. Tangu serikali yake ilipoanza kupokea maombi ya ukimbizi 1994, imewatambua wakimbizi 175 na kuwapa hadhi ya hifadhi ya kibinadamu wengine 93 ambao walibainika kuwa sio wakimbizi lakini wanahitaji kulindwa kimataifa.

Tangu mwaka 1994 hadi mwishoni mwa mwaka 2009 Jamuhuri ya Korea imepokea maombi ya ukimbizi karibu 2500 na mengine 321 yanasubiri kushughulikiwa.