Silaha bado zinauzwa Afrika kinyemela

Silaha bado zinauzwa Afrika kinyemela

Licha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa silaha bado zinaingizwa kinyemela katika maeneo ya vita Afrika. Taarifa iliyowasilishwa kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na Rosemary A Dicarlo mwakilishi wa Marekani kwa masuala ya kisiasa ya uingizaji haramu wa silaha Afrika ya Kati inasema kila mwaka maelfu ya silaha ya thamani ya mamilioni ya dola yanaingizwa kinyemela katika maeneo yenye migogoro barani Afrika.

Amesema hatua hii inaendelea licha ya vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa. Ameongeza kuwa kuingia huko kwa silaha kuna maanisha vifo kwa maelfu ya watu, mamilioni kuwa wakimbizi wa ndani na wengine kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi sehemu zingine.

Na idadi ya wakimbizi inapoongezeka inamaana kuwa mabilioni ya dola yanatumika katika kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi hao. Hali hii inawasikitisha sana nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Takwimu zilizokusanywa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba vita vinavyochechewa na biashara haramu ya silaha vimewasababisha watu milioni 14 kuzikimbia nyumba zao na kuwa wakimbizi kote duniani. Wengine milioni 26 wamekuwa wakimbizi wa ndani.

Hali ya kutokuwa na amani na usalama inayochangiwa na vita hivyo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo, na Afrika ndio muathirika mkubwa wa hali hii. Katika nchi 20 masikini kabisa duniani zote isipokuwa moja tuu ni za Afrika. Na nyingi zimepitia vita tangu mwaka 1990 na mfano mzuri ikiwa ni Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo imechangia msukosuko pia katika eneo lote la maziwa makuu.

Kimsingi usalama mdogo na umasikini usiokwisha Afrika ya Kati na kwengineko kuliko na vita na migogoro kumechangiwa sana na biashara ya silaha, na hivyo kufanya juhudi za kitaifa na kimataifa za kuleta maendeleo kuwa ngumu.