Israel imefunga ukingo wa magharibi kwa saa 48 kuzuia wapalestina kuingia
Israel imefunga mpaka wa Ukingo wa Magharibi ili kuwazuia Wapalestina wasiingie Israel wakihofia kuzuka kwa ghasia. Kumekuwa na mapigano baada ya sala ya leo Ijumaa katika miskiti mbalimbali mjini Jerusalem na kwengineko pia ghasia zimekuwepo wiki nzima hii.
Ghasia hizo zimechagizwa na kukwama kwa mazungumzo ya amani na Israel kuingia bila ridhaa katika maeneo mawili matakatifu kwa Wapalestina kwenye ukingo wa Magharibi.
Hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu Ban Ki-moon amelaani mipango ya Israel ya kutaka kuongeza makazi ya Walowezi na kusema inakinzana na sheria za kimataifa.
Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Riyad Mansour ameielezea hatua hiyo ya Israel kama ni uchokozi na amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulishughulikia suala hilo mara moja.