Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa kimataifa wahitajika kukomesha ukatili dhidi ya wanawake

Ushirikiano wa kimataifa wahitajika kukomesha ukatili dhidi ya wanawake

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ukatili dhidi ya wanawake unaharibu kabisa maisha ya watu na kuacha athari kubwa kwa jamii.

Leo ametoa wito wa kuwepo na umoja wa kuchukua hatua kukabiliana na ukatili huo na wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria. Amesema kila palipo na visa vya unyanyasaji wa wanawake, usafirishaji haramu wa wanawake kutumika katika biashara ya ngono, mauji yatokanayo na mila na ukeketaji, ukatili dhidi ya wanawake na wasichana unaendelea na hilo ni kosa la jinai.

Bwana Ban ameyasema hayo katika mjadala kuhusu ukatili dhidi ya wanawake kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York. Ameongeza kuwa mbali na ukatili huo kuharibu maisha binafsi ya wanawake wengi, pia unarudisha nyuma maendeleo, unasababisha mtafaruku na kufanya amani ime kazi ngumu kuipata.

Amesema wote tunahitaji kuungana na kudai mkono wa sheria kuwajibika juu ya suala hili, ili wanawake na wasichana wasipokonywe haki zao. Wote tunahitaji kuchukua hatua madhubuti kukomesha ukatili huu. Ni lazima tusikilize na kuwasaidia waathirika. Lazima tushughulikie kiini cha ukatili dhidi ya wanawake kwa kutokomeza ubaguzi na kubadili mtazamo wa watu .