Skip to main content

Dola milioni 123 zahitajika kuisaidia Nepal

Dola milioni 123 zahitajika kuisaidia Nepal

Mashirika ya misaada yametoa wito wa kupata dola milioni 123 kuwasaidia watu nchini Nepal. Fedha hizo zitafadhili miradi ya kuwasaidia zaidi ya raia milioni tatu kwa msaada wa kuokoa maisha yao ikiwa ni pamoja na chakula kwa mwaka mzima.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu OCHA imebaini kuwa karibu nusu ya wilaya za Nepal zinakabiliwa na upungufu wa chakula na watu takribani milioni 2.5 hawana uhakika wa kuwa na chakula.

Zaidi ya hayo Nepal iko katika hatari ya majanga asilia kama mafuriko, maporomoko ya ardhi na matetemeko ya ardhi. OCHA inasema kuimarisha maandalizi na mfumo wa kuwatahadharisha watu ni mambo ya kupewa kipaumbele.

Ombi hilo la msaada wa fedha pia utaisaidia Nepal kuimarisha mfumo wake wa maandalizi na kutoa tahadhari za majanga. Nchi hiyo inawahifadhi pia wakimbizi wapatao elfu 89 kutoka nchi jirani ya Bhutan.