Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ki-moon awataka Watogo kufanya uchaguzi kwa amani

Ban ki-moon awataka Watogo kufanya uchaguzi kwa amani

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amesema kwamba uchaguzi mkuu wa Rais utakaofanyika wiki hii nchini Togo ni fursa nzuri kwa nchi hiyo kuendeleza juhudi za kuleta demokrasia.

Bwana Ban ametoa wito wa uchaguzi huo kufanyika kwa amani bila ghasia zozote. Uchaguzi huo utakaofanyioka tarehe 4March pia unatoa nafasi ya kudumisha umoja wa kitaifa, kudumisha utulivu na kuleta maendeleo ya nchi.

Ametoa wito pia kwa taasisi na viongozi wote wa kisiasa nchi humo kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki na unakumbatia matakwa ya watu wa Togo, na amezitaka jumuiya zote za kiraia kuepuka hatua zozote zitakazochochea ghasia.

Ameahidi pia msaada wa umoja wa Mataifa katika mchakato mzima wa uchaguzi wan chi hiyo ya Afrika ya magharibi. Mamia ya watu walikufa na wengine kwa maelfu kujeruhiwa kufuatia ghasia zilizozuka baada ya aliyekuwa Rais wa muda mrefu wan chi hiyo Gnassingbe Eyadema kufariki ghafla na kufanyika uchaguzi ulioghubikwa na utata mwaka 2005. Maelfu ya raia wa Togo walikimbilia nchi jirani za Ghana na Benin mwaka huo kuepuka ghasia.