UM watathmini hali ya Chile na kuanza kutoa msaada

UM watathmini hali ya Chile na kuanza kutoa msaada

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu OCHA imesema tathmini yao ya awali inaonyesha kuwa watu milioni mbili wameathirika na tetemeko la ardhi lililoikumba Chile na wengine 723 wamefariki dunia.

Pia tetemeko hilo kwa mujibu wa OCHA limeharibu nyumba milioni moja nukta tano. Na ofisi ya kitengo cha dharura cha taifa cha Chile ndicho kinachoratibu shughuli za misaada. Shirika la afya duniani WHO kwa upande wake linasema huduma za afya nchini humo zinaendelea kupatikana kutokana na mahitaji.

Lakini tatizo linaloikumba Chile kwa sasa ni kuweza kuwa na utaratibu wa huduma ya mfululizo ambayo haitoweza kuingiliwa . Hospitali katika jimbo la Metropolitan uliko mji wa Santiago zinafanya kazi, lakini eneo lililoathirika zaidi na tetemeko la ardhi hospital nane hazifanyi kazi na zingine kumi zimeharibiwa vibaya na zinahitaji kuchunguzwa kabla ya kuendelea kutoa huduma.