UM waitaka Misri kuacha kutumia nguvu dhidi ya wahamiaji

UM waitaka Misri kuacha kutumia nguvu dhidi ya wahamiaji

Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Navi Pillay leo ametoa wito kwa serikali ya Misri kuamuru mara moja vikosi vyake vya usalama kuacha kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wahamiaji wasiokuwa na silaha, ambao wanajaribu kuingia Israel kupitia jangwa la Sinai.

Hatua hiyo imekuja baada ya taarifa za visa vya watu 60 kuuawa kwa kupigwa risasi katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita.

Bwana Pillay amesema wahamiaji wengi na watu wanaotafuta hifadhi za ukimbizi hukutana na matatizo mengi na wengi wao wanatoka kusini mwa jangwa la Sahara hususani Eritrea, Ethiopia na Sudan.

Mwaka huu pekee wahamiaji tisa wameuawa na vikosi vya Misri wakijaribu kuingia Israel. Robert Kolvin ni msemaji wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.