Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yataja majina 20 ya waliohusika na machafuko Kenya

ICC yataja majina 20 ya waliohusika na machafuko Kenya

Kufuatia ombi la maelezo zaidi mapema mwezi huu kutoka mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC iliyoko The Hague Uholanzi, waendesha mashitaka wake wametaja majina ya watu 20 wanaodai walihusika na ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya.

Ghasia hizo zilizozuka mwezi Desemba 2007 hadi Januari 2008 zilikuwa na misingi ya kikabila na zilisababisha vifo vya watu 1000 na wengine laki tatu kuzikimbia nyumba zao. Mwezi Novemba mwaka jana Luis Moreno-Ocampo aliomba ridhaa ya kitengo cha kesi ili kuanza uchunguzi wa ghasia hizo ambazo zilitokea kutokana na matokeo ya uchaguzi yaliyokuwa na utata yaliyompa Rais Mwai Kibaki wa PNU ushindi dhidi ya mpinzani wake kutoka ODM Raila Odinga ambaye sasa ni waziri mkuu.

Mr. Moreno-Ocampo amesema maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa na wafanya biashara kutoka vyama hivyo viwili PNU na ODM waliandaa, kuchochea na kufadhili mashambulizi dhidi ya raia kutokana na misingi yao ya kikabila au vyama wanavyoviunga mkono. Majina ya watu hao 20 ambao waendesha mashitaka wanaamini wanabeba jukumu la mauaji hayo, kwa sasa yamefungwa katika bahasha.

Majina hayo yamepatikana baada ya kuwahoji watu wengi waliojeruhiwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan akayakabidhi majina hayo kwa bwana Moreno-Ocampo mapema mwaka jana.Bwana Ocampo ameongeza kuwa kama majaji wataidhinisha uchunguzi atawahusisha wale ambao watataka kutoa maelezo kuhusu kuhusika kwao au taarifa zaidi, na amekikumbusha kitengo cha kesi kuwa hakuna hata mtu mmoja kati ya hao 20 ambaye amefunguliwa mashitaka nchini Kenya kutokana na uhalifu huo.

Kwa sasa majina hayo ni kama ishara tuu amesisitiza mwendesha mashitaka, na kudai kuwa madai dhidi ya majina yaliyotajwa lazima yaambatane na ushahidi utakaokusanywa na ofisi ya mwendesha mashitaka.