Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID imepoke helikopta tano kutoka Ethiopia

UNAMID imepoke helikopta tano kutoka Ethiopia

Mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na ule wa Afrika kwenye jimbo la Darfur Sudan UNAMID, leo umepokea rasmi helkopta tano kutoka Ethiopia ili kusaidia katika shughuli zake za kulinda amani.

Helkopta hizo zilizotengenezwa Urusi ambazo zimesubiriwa kwa muda mrefu zimekabidhiwa kwa UNAMID katika shehere iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali ya Sudan, UNAMID na nchi jirani ya Ethiopia kwenye eneo la Nyala Kusini mwa Darfur.

Mwakilishi maalumu wa UNAMID Profesa Ibrahim Gambari amesema ameridhika kupokea helkopta hizo kwa niaba ya mpango mzima wa kulinda amani. Ameongeza kuwa helkopta hizo zitauwezesha mpango wa kulinda amani kuwalinda raia na kusaidia haraka katika hali ya dharura.

Amesema pia helkopta hizo zitaongeza imani ya wanachi kwa UNAMID hasa ya kuwalinda na anatumai zitawaogopesha wale wanaotishia amani na usalama wa jimbo la Darfur.

Naye mwakilishi wa kudumu wa Ethiopia kwenye Umoja wa Afrika Konjit Sinegiorgis aliyeongoza jopo la Ethiopia kwenye hafla hiyo , ambalo lilijumuisha zaidi maafisa wa jeshi, akizungumza katika hafla hiyo amesema amefurahishwa na mapokezi na hafla yenyewe lakini amesisitiza kuwa haja ya majadiliano ya kisiasa ipo ili kumaliza mzozo wa Darfur.