Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa yuko Chad kuzungumzia ombi la kuondoa vikosi

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa yuko Chad kuzungumzia ombi la kuondoa vikosi

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kulinda amani Alain Le Roy amewasili nchini Chad kwa ajili ya mazungumzo, kufuatia ombi la serikali mjini Ndjamena la kutaka vikosi vya Umoja wa Mataifa viondoke nchini humo.

Bwana Le Roy atakuwepo Ndjamena hadi Jumatatu ijayo na siku ya Jumapili atakwenda katika eneo la Abeche mashariki mwa nchi hiyo ambako kuna maakao makuu ya vikosi vya UM vya kulinda amani Jamuhuri ya Afrika ya Kati na Chad vijulikanavyo kama MINURCAT. Vikosi hivyo pia vina makao nchini Jamhuri ya afrika ya Kati, ambako vinasaidia kulinda wakimbizi na watu waliotawanywa na vita, lakini serikali ya Chad inasema vikosi hivyo vinashindwa kutimiza wajibu wake.

Wakati wa ziara yake Le Roy atazungumza na waziri wa mambo ya nje wanchi hiyo, Mwakilishi wa Rais Idris Deby kwa mpango huo wa MINURCAT na waziri mkuu. Lakini pia ikiwezekana atakutana na Rais Idris Deby.