Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda itakuwa mwenyeji wa sherehe za 'Siku ya Mazingira' mwaka 2010

Rwanda itakuwa mwenyeji wa sherehe za 'Siku ya Mazingira' mwaka 2010

Shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP leo limetangaza kwamba Rwanda itakuwa mwenyeji wa kimataifa wa sherehe za mwaka huu wa 2010 za siku ya mazingira duniani, zinazoazimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni.

UNEP imeuchagua mji mkuu wa Rwanda Kigali kama kitovu cha sherehe hizo kwa sababu ya manzari yake mazuri kimazingira ikiwa pia na viumbe hadimu kama sokwe wa milimani na pia juhudi zake za kuchagiza maendeleo ya uchumi yanayojali mazingira.

Agenda ya siku hiyo kwa mwaka huu itakuwa "viumbe vingi, sayari moja, na aina moja ya maisha ya siku za usoni."

Rwanda ni nchi ya Afrika ambayo licha ya changamoto kubwa inakumbatia fursa zinazopatikana kuwa na uchumi unaojali mazingira , amesema Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Achim Steiner.

Nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki inayojulikana kama nchi ya milima elfu moja , inajikita katika mikakati endelevu ya mazingira kama kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, kuchagiza kampeni za masuala ya usafi unaotunza mazingira, kutenga eneo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi nyani, na kuanzisha miradi ya matumizi ya nishati ya jua na bayoanuai, imesema UNEP.