Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi ya Kiongozi wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, anaye shikiliwa nchini Sierra Leone inaendelea

Kesi ya Kiongozi wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, anaye shikiliwa nchini Sierra Leone inaendelea

Makala yetu ya wiki leo inazungumzia kesi ya aliyekuwa Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor ambaye kwa sasa anazuiliwa nchini Sierra Leone.

Charles Taylor anashutumiwa kwa kufadhili na kusaidia makundi ya waasi yaliyo na hatia ya kutekeleza mauji nchini Sierra Leone wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe , kwa kubadilishana na hisa kwenye biashara ya almasi. Bwana Taylor anakana mashitaka yote,lakini pasipo na matumaini. Joseph Kamara naibu mwendesha mashitaka katika mahakama ya uhalifu inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone anafafanua kuhusu kesi hiyo

JOSEPH KAMARA: "Tumekusanya Ushahidi ambao tumeuwasilisha mbele ya mahakama na unasaidia , tumeridhika na ushahidi huo kwa sababu kitu cha muhimu tulitakiwa kuthibitisha kuwepo kwa uhusiano baiana ya Taylor na vitendo vilivyokuwa vikitendeka Sierra Leon, kwa sababu hatukumshitaki kwa makosa nchini Liberia, na kwamba kwa kiasi kikubwa tumeweza kuthibitisha ushahidi wetu mbele ya mahakama. Tuliwaleta watu wake wa karibu, aliofanya nao kazi, makamanda wenzie wakati alipokuwa akitoa baadhi ya amri ambazo zilitekelezwa wakati wa vita vya Sierra Leone. Hivyo tuliwaleta mashahidi wote hao mahakamani ,tulilidhika kabisaa na ushahidi na ni ushahidi mzito."

NUBA ELAMIN:Pamoja na kwamba upande huo wa mshitaka umefanikiwa kuwaleta mashahidi wote hao mbele ya mahakama mjini The Hague ilikuwa kazi rahisi au walikabiliana na vikwazo gani?

JOSEPH KAMARA: "Bila shaka ndio kuna matatizo kidogo yaliyojitokeza kama kuwahamisha mashahidi kutoka sehemu moja kwenda nyingine ,hususani ambapo mashahidi hawa ni huenda hawajawahi kusafiri kabisa hapo kabla katika maisha yao, na siku zote huwa kunakuwa na hofu inayowaghubika, hivyo tumekuwa na msaada kwa mashahidi mahakamani ambao umekuwa ukitusaidia kuwaleta watu hawa, sio tu kwa wao kuja na kutoa ushahidi pia kuwaandaa na kwa kesi. Hivyo kumekuwa na matatizo kadhaa ya kiufundi kuhusiana na idadi na tukalazimika kupunguza idadi ya mashahidi, lakini kama ambayo kila wakili anavyofahamu , sio idadi ya mashahidi ambayo inaipa uzito kesi yako, ni uzito wa ushahidi wakati unapouwasilisha, na tuanridhika na uzito huo."

NUBA ELAMIN: Haya ushahidi umeshawasilishwa na watetezi wameshatetea kesi yao, nini hasa kinachoendelea kwa sasa katika kesi hiyo ya Charles Taylor?

JOSEPH KAMARA: "Tumemaliza kumuhoji ,tumemkabili na masuala kama ya akaunti zake pale alipojaribu kujitetea kuwa yeye ni mtu wa kawaida na hana pesa. Tulimkabili na ushahidi kutoka kwa Citibank ukionyesha mamilioni ya dola yaliyohifadhiwa. Pia tumemkabili na taarifa zinazohusu matumizi ya askari watoto, kwa upande wake amewaelezea kama boy scouts, lakini kwetu sisi tunajua ni kuwafunza askari watoto na aliafiki. Kwa kiasi kikubwa tumeridhika na majibu aliyotupa na pia inaonyesha dhahiri kiwango cha mauaji tunayoyaangalia."

NUBA ELAMIN:Ukiachia mbali mauji ya kikatili yaliyofanyika na kuwashirikisha watoto vitani ,Taylor anashutumiwa kwa kujihusisha na biashara haramu ya almasi, je hili nalo limepewa uzito katika kesi yake? Bwana Kamara anafafanua.

JOSEPH KAMARA: "Sehemu ya kesi ya waendesha mashitaka ni kwamba nia ya kujihusisha na mgogoro wa Sierra Leone ilikuwa ni kuongeza mapato ya kusaidia malengo yake nchini Liberia na eneo zima kwa ujumla ,na chanzo cha mapato hayo ni almasi. Na almasi hizo zimebatizwa kuwa ni almasi za damu kwa sababu chanzo chake ni eneo la vita, na kesi ni kwamba kutafuta almasi hizi ilikuwa ni kujipatia mapato,ili aweze kuruka maazimio ya Umoja wa Mataifa na kuweza kupata silaha na risasi kusaidia vita nchini Liberia na vita nchini Sierra Leone, hivyo ni kesi nzito kwa waendesha mashitaka , tunaweza kuongoza kwa ushahidi."

NUBA ELAMIN:Lakini bado swali linasalia yote hayo tumeyasikia kesi na mashitaka yanayomkabili Charles Taylor , ushahidi uliotolewa na uzito wa kesi yenyewe. Nini sasa kitakachofuata na lini kesi hii itafikia tamati? Kwa mujibu wa bwana Kamara hivi sasa mpira wote uko mikononi mwa upande wa utetezi,ambao inasemekana wanaangalia upya idadi ya mashahidi na huenda wakawapunguza. Kesi hii ya Charles Taylor imekuwa na mvuto mkubwa sio tuu nchini Liberia anakotoka au Sierra Leon aliko sasa bali sehemu mbalimbali duniani imekuwa ikifuatiliwa, wakiwemo viongozi wa bara la Afrika.Je imewapa funzo lolote kesi hii? Kwa mujibu wa Kamara funzo la kwanza la kujifunza ni kwamba hakuna mtu yoyote aliye juu ya sheria hata kama alikuwa Rais, na jambo lingine ni kwamba wote tunajifunza kuishi kwa kuzingatia mfumo wa sheria."

Nikiripotia redio ya Umoja wa Mataifa kutoka New York mimi ni Nuba Elamin.