Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya UM yamuhuku kifo cha miaka 15 askari wa zamani wa Rwanda

Mahakama ya UM yamuhuku kifo cha miaka 15 askari wa zamani wa Rwanda

Mahakama ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kesi za mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, leo imemuhukumu kwenda jela miaka 15 askari wa zamani wa chi hiyo ikimkuta na hatia ya kuchochea na kushiriki moja kwa moja kwenye mauaji ya kimbari.

Uamuzi wa leo dhidi ya Tharcisse Muvunyi unafuatia hukumu ya pili baada ya awali kukutwa na hatia ya makosa kadhaa ikiwemo kuchochea na kushiriki moja kwa moja kuichagiza jamii kufanya mauaji ya kimbari, na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu na kuhukumiwa kwenda jela miaka 25 na mahakama hiyo ya ICTR iliyoko Arusha Tanzania mwaka 2006.

Mwaka 2008 kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo kiliweka kando hukumu na kifungo alichokuwa amepewa na kikaagiza kesi ifanyike upya, na kesi ikaanza tena mwezi June mwaka jana ikiwa na kosa moja la kuchochea na kuchagiza jamii kushiriki mauaji ya kimbari kutokana na hotuba aliyoitoa bwana Muvunyi mjini Butare mwezi May 1994, ambapo alitoa wito wa kuwaua Watusi ambao yeye alikuwa anawaita nyoka.

Bwana Mvunyi mwenye miaka 57 alikuwa luteni kanali kwenye jeshi la Rwanda. Alikamatwa nchini Uingereza mwaka 2000 na kuwekwa kwenye kizuizi cha Umoja wa Mataifa na baadaye akahamishiwa kwenye mahaka ya ICTR iliyoko Arusha Tanzania baadaye mwaka huohuo.

Baraza la usalama liliidhinisha kuundwa kwa mahakama hiyo mwishoni mwa mwaka 1994 ili kukabiliana na kesi za mauaji ya kimbari ambayo yalikatili maisha ya watu takribani laki nane, wengi wao wakiwa Watusi na Wahutu wenye msimamo wa wastani. Wengi waliuawa kwa kukatwa mapanga katika kipindi cha siku 100 kuanzia mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huo 1994.