Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya chanjo Somalia yawafikia watu laki sita

Kampeni ya chanjo Somalia yawafikia watu laki sita

Nchini Somalia licha ya mapigano yaliyowasambaratisha maelfu wa watu mjini Moghadishu,wafanyakazi wa afya wameweza kuruka viunzi mjini Moghadishu katika kampeni ya miezi mitatu iliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na kufanikiwa kutoa chanjo Kwa wanawake laki tatu wenye umri wa kuweza kuzaa na watoto 288,000.

Watoto walipewa chanjo ya polio, surua, kikohozi na pepo punda, na pia waligawiwa tembe za vitamin A,za kutibu minyoo na pia kupimwa kiwango cha lishe. Wakati wanawake kwa upande wao walipata chanjo ya pepo punda, katika kampeni hiyo ya afya ya mtoto iliyofadhiliwa pia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la afya duniani WHO.

Chanjo hiyo ni sehemu ya juhudi za kampeni ya nchi nzima ya kutoa huduma ya afya itakayookoa maisha ya kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano na kila mwanamke mwenye umri wa kuweza kuzaa. Licha ya mafanikio waliyopata hata hivyo Dr Imran Raza Nirza wa UNICEF anasema kampeni hiyo ilikumbwa na misukosuko.