Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa kidini wanawake wapambana na ukimwi

Viongozi wa kidini wanawake wapambana na ukimwi

Viongozi wa kidini wanawake wameamua kuchukua jukumu kubwa la kuongoza vita dhidi ya ukimwi nchini Somalia.

Hatua hii imekuja kutokana na mafufunzo yanayoendeshwa na mashirika mbalimbali yanayofadhiliwa na shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP.

Somaliland UNDP imesaidia kutolewa mafunzo mara nne kwa wanawake viongozi wa kidini mjini Hargeisa, Borama, Berbera na Buroa kwa kushirikiana na mtandao wa Somaliland wa masuala ya virusi vya HIV na ukimwi. Na hivyo kuwaweka wanawake msitari wa mbele katika uhamasishaji na utoaji elimu katika jamii.

Kwa kutumia mfumuo wa programu ulioandaliwa na UNDP kwa mataifa ya Kiarabu ,wanawake hao viongozi wa dini wameelimishwa masuala muhimu, hasa mila potofu ambazo zinachangia kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa huo, unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi. Na jukumu la muhimu ni kwamba viongozi wa dini na jamii kusaidia kupunguza idadi ya maambukizo mapya ya HIV na pia kusaidia wagonjwa.

Viongozi hao pia mbali ya nyenzo walipewa ujumbe kutoka katika kitabu kitakatifu cha Koran ambao unachagiza mapambano dhidi ya virusi vya HIV na ukimwi. Mafunzo hayo yanasaidia kutoa kauli moja ya kuzuia, kutibu ,kuwahudumia na kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya HIV, ujumbe ambao utazambazwa kwa watu siku ya swala ya Ijumaa.

Utamaduni na dini ni vitu vilivyo na uhusiano mkubwa katika jamii ya Kisomali. Hivyo viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuongoza vita dhidi ya ukimwi na kupigia upatu kusaidiana kubeba jukumu kukemea tabia na mwenendo unaochangia kuenea kwa ukimwi.

Majadiliano yao ya wazi na waumini wao yatasaidia kuwapasha taarifa na kuwaelimisha waumini na kuwatia moyo wa kuyakubali mabadiliko mazuri licha ya kwamba suala lenyewe ni nyeti na linahusiana na masuala ya ngono, jambo ambalo si rahisi kujadiliwa mara kwa mara na jamii.

Mafunzo hayo ymehudhuriwa na wanawake viongozi wa dini zaidi ya 100 kutoka sehemu mbalimbali za Somaliland. Hadi kufikia Desemba mwaka jana zaidi ya viongozi 800 wa kidini wamepatiwa mafunzo na kuwapa uwezo viongozi hao kuwa wajumbe wa kuleta mabadiliko katika kukabiliana na virusi vya HIV na ukimwi.