Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Askari watoto waendelea kuachiliwa nchini Chad

Askari watoto waendelea kuachiliwa nchini Chad

Hatua ya hivi karibuni ya kuendelea kuwaachilia askari watoto wanaoshiriki vita kaskazini magharibi mwa Chad ,inafanya idadi ya watoto wanaorejeshwa katika maisha ya kawaida tangu mwaka 2009 kufikia 240.

Walioachiliwa hivi karibuni ni watoto wenye umri wa kati ya miaka 11 na 18, na watoto wote 15 walioachiliwa walihamishwa na kutoka mjini Moussoro na kupelekwa kwenye vituo vya muda vinavyosimamiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, shirika la CARE international na kusaidiwa na UNICEF kwenye mji mkuu wa Chad N'djamena. Katika vituo hivyo vya muda watakaa kwa miezi mitatu wakati juhudi zikifanyika kuwarejesha kwenye maisha ya kawaida.

UNICEF hivi sasa inasaidia vituo viwili mjini N'djamena ambavyo kila kimoja kina uwezo wa kuhifadhi watoto 100 .Vituo hivyo vinaendesha shughuli mbalimbali na kutoa msaada kwa vijana hao ili waweze kurejea katika maisha ya kawaida. Miongoni mwa vitu wanavyopata ni chakula, huduma za afya, na ushauri nasaha, ikiwa ni pamoja na elimu na mafunzo ya aina mbalimbali kama uwashi.