Viongozi wa Afrika washikamana kusaidia kuzuia malaria
Viongozi wa Afrika wanaokutana nchini Ethiopia kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika unaojadili changamoto zinazolikumba bara hilo, hasa juhudi za kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa , leo wamejadili suala la kukabiliana na malaria.
Wakuu wa nchi 26 wamejadili suala hilo katika kikao cha muungano wa viongozi wa Afrika wa kukabiliana na malaria (ALMA) kwenye mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Afrika unaofanyika mjini Addis Ababa. ALMA inalenga kuutokomeza ugonjwa wa malaria ambao unasababisha asilimia 25 ya vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano barani Afrika na kuathiri zaidi ya mama wajawazito milioni 50. Malaria ndio chanzo cha asilimia 10 ya vifo vyote vya watoto na kina mama wajawazito.
Nchi hizo 26 za muungano wa ALMA zinasema katika kipindi cha miezi 12 iliyopita pekee , vyandarua vya mbu takribani milioni 90 vimepelekwa barani Afrika , na kwa jumla vyandarua milioni 200 vimegawanywa kwa watu milioni 400 katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara, ambako vifo vingi vinavyotokana na malaria vinatokea.