Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake yazinduliwa

Kampeni ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake yazinduliwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, mwishoni mwa juma ametoa wito wa kuungwa mkono na viongozi wa Afrika katika kampeni yake ya kumaliza ukatili dhidi ya wanawake uliomea mizizi katika bara hilo. Ambao amesema ni kikwazo kikubwa cha maendeleo barani humo.

Amesema "tunajua wanawake wa Afrika ndio walio mstari wa mbele katika kuziweka pamoja familia, jamii zao na taifa kwa ujumla." Bwana Ban ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo iitwayo "Tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake" mjini Addis Ababa Ethiopia.

Wanawake wa Afrika ndio chachu katika kuushinda umasikini, kumaliza tatizo la njaa, kupambana na ujinga, kuponya wagonjwa, kuzuia kuenea kwa maradhi na kuleta amani na utulivu" Amesema bwana Ban.