Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya watu walokimbia makazi Yemen imepindukia 250,000

Idadi ya watu walokimbia makazi Yemen imepindukia 250,000

Hali ya mzozo wa kibinadamu huko Yemen ikendelea kuzorota, Idara ya kuwahudumia wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR ilitangaza Ijuma kwamba inakadiria watu 250, 000 wamekimbia makazi yao tangu mapambano kuzuka nchini humo 2004.

Mnamo wiki sita zilizopita kiasi ya watu elfu 7 wamekua wakikimbilia jimbo la Hajjah kila wiki kutokea jimbo la Sa'ada huko kaskazini mwa nchi ambako kumezuka mapigano mepya kati ya vikosi vya serekali na waasi wa Al Houthi.

Msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic aliwaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba mapigano yamesonga mbele kutoka mji wa Sa'ada na kuenea hadi huko kaskazini magharibi ya nchi, akiongeza kwamba sababu nyingine ya watu kukimbia ni kutoweza tena kumudu maisha katika jimbo hilo la Sa'ada.

Ingawa makambi matatu kwa ajili ya watu walopoteza makazi yao katika jimbo jirani la Hajjah yanaendelea kupanuliwa, UNHCR ina wasi wasi hata hivyo kutokana na ukosefu wa hema, kwani watu wengi walokimbia wanaonekana wakishi katika katika maeneo yanayojitokeza kiholela kando kando ya barabara zinazoelekea kwenye makambi hayo.