Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama linaongeza muda wa vikosi vya UM nchini Cote d'Ivoire

Baraza la Usalama linaongeza muda wa vikosi vya UM nchini Cote d'Ivoire

Baraza la Usalama limeidhinisha Alhamisi, kuongeza muda wa afisi ya Umoja wa Mataifa nchini Cote d\'Ivoire, UNOCI pamoja na ule wa vikosi vya Ufaransa vinavowasaidia, kwa miezi minne zaidi ili kusaidia kuandaa uchaguzi wa huru, haki na wazi katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Hapo mwanzoni uchaguzi ulipangwa ufanyike mwaka 2005, lakini umeahirishwa mara kwa mara, na hivi sasa umepangwa kufanyika mwezi Marchi. Kwa sauti moja baraza liliidhinisha azimio linalowahimiza viongozi wanaohusika huko Cote d'Ivoire kuhakikisha wanachapisha orodha ya mwisho rasmi ya wapiga kura, kutangaza tarehe rasmi ya duru ya kwanza ya uchaguzi na kutekeleza ahadi zao kwa ukamilifu. Katika kuimarisha usalama kabla ya uchaguzi, wajumbe 15 wa baraza walieleza nia ya kuongeza idadi ya wanajeshi 7 450 wa UNOCI kwa wanajeshi 500 zaidi kwa kipindi kifupi.

Wiki iliyopita mjumbe maalum wa Katibu mkuu huo Cote d'Ivoire, Choi Young-Jin, aliliambia Baraza la Usalama kwamba kuchapishwa kwa orodha ya muda ya wapiga kura mwezi Novemba ilikua miongoni mwa mafanikio makubwa katika miezi ya hivi karibuni kuelekea uchaguzi.

Wakati huo huo alitaja baadhi ya masuala yaliyobaki kutanzuliwa ikiwa ni pamoja na kuliunganisha tena taifa hilo lililogawika mapande mawili, kaskazini ikishikiliwa na waasi na serekali kushikilia maeneo ya kusini, tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe 2002.

Baraza la Usalama liliidhinisha halikadhalika, kuongeza kwa mwaka mmoja zaidi muda wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM, na kuhimiza kuongezwa nguvu zake kufikia wanajeshi elfu 8.