Skip to main content

Mjumbe wa UM na Umoja wa Afrika amejadili Darfur na viongozi wa Sudan

Mjumbe wa UM na Umoja wa Afrika amejadili Darfur na viongozi wa Sudan

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, Ibrahim Gambari, amekutana na waziri wa ulinzi wa Sudan kujadili mustakbal wa eneo la Darfur linalokumbwa na ghasia, kama sehemu ya mikutano kadhaa na viongozi wa Sudan .

Bw Gambari ambae alichukua wadhifa wake hivi karibuni kama mkuu wa afisi ya pamoja ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa na AU, alikutana Ijumatano mjini Khartoum na Jenerali Abdelrahim Mohamed Hussein, na kueleza kuridhika kwake na jinsi alivyopokelewa na serekali na wananchi wa Sudan. Alisema atafanya kila awezalo kuhamasisha amani na ustawi wa kudumu huko Darfur ambako UNAMID imekua ikijaribu kusitisha ghasia za Darfur tangu 2007. Ghasia zinazoaminika zimesababisha vifo vya karibu watu laki tatu na wengine milioni 2.7 kupoteza makazi yao tangu vita kuanza 2003.

Bw Gambari amesema atafanya kazi kuhakikisha majukumu ya UNAMID yanafanyika kwa njia ya usawa kabisa, bila ya upendeleo na kwa uwazi. Waziri wa ulinzi kwa upande wake alisema kwamba, serikali itasaidia kazi za mjumbe mpya. Mkutano wao ulizingatia pia uhusiano kati ya Sudan na Chad na maafisa hao wawili waliahidi kufanya kazi kwa karibu katika kutekeleza mkataba ulofikiwa mwaka jana baina ya nchi hizo jirani.