Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni lazima juhudi za kuikarabati Haiti ziimarishe Haki za Binadamu

Ni lazima juhudi za kuikarabati Haiti ziimarishe Haki za Binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, katika juhudi za kujenga upya miundo mbinu ya Haiti kufuatia tetemeko la ardhi, ni lazima kuzingatia kuimarisha mfumo wa haki za binadamu nchini humo.

Taarifa ya Bi Navi Pillay kwa kikao maalum cha Baraza la Haki za Binadamu juu ya Haiti, inaeleza kwamba ni lengo lao kuhakikisha kwamba wananchi wa Haiti wanapata heshima na haki zao zote. Alisema Idadi kubwa ya wa-Haiti wako hatarini kukabiliwa na ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na ubaguzi kutokana na kiwango kikubwa cha umaskini. Alisema ni lazima kuweka utaratibu kuzuia na kupunguza ukiukaji ambao mara nyingi hutokea baada ya maafa makubwa. Akisoma taarifa ya Pillay, naibu kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Kyung-wha Kang alisema:

Kufikia lengo hili, usimamizi mkali unahitajika ili kuwalinda wale ambao wako hatarini zaidi, hasa walemavu na watu wazee, maskini, wanawake na watoto ambao huwenda wakakabiliwa na hatari za kukamatwa kiholela, ghasia, zikiwa ni pamoja na zile za ngono na biashara haramu ya kusafirisha binadamu. Ninawahimiza wote wanaohusika kuitikia mwito wa UNICEF na kutoacha juhudi zozote katika kuwaunganisha watoto na familia zao binafsi. Kuna hofu kwamba wafungwa, ambao walikimbia kutoka jela za Haiti ikiwa ni pamoja na wale wahalifu sugu wa magengi, huwenda wakapata silaha na kuanza uhalifu wa utumiaji nguvu. Ni lazima kurudishwa kwa haraka utawala wa kisheria.

Kufuatia maafa hayo, Haiti ililiomba Baraza la Haki za Binadamu kuahirisha uchunguzi wa rikodi yake ya haki za binadamu ulotarajiwa kufanyika mwezi May mwaka huu.