Skip to main content

Huduma za dharura zinaimarika Haiti

Huduma za dharura zinaimarika Haiti

Afisi ya Idara ya Umoja wa Mataifa juu ya Misaada ya Dharura OCHA imeeleza kua kazi za kuratibu huduma huko Haiti zinaimarika siku hadi siku. Kituo kipya cha pamoja cha kuratibu na kuongoza kazi kimepewa jukumu la kuhakikisha usalama wa kuwasilisha msaada wote wa dharura.

Hema zinahitajika sana kuweza kuwapatia watu makazi ya muda hasa kutokana na msimu wa mvua unaotarajiwa kuanza mwezi wa April, imesisitiza OCHA.

Idara ya Chakula Duniania WFP inasema, imeshawafikia karibu watu laki nne na nusu kwa kuwapatia chakula cha kila siku, na imeajiri malori 75 yanayosafirisha chakula kutoka Jamhuri ya Dominica.

UNICEF inasema vituo 115 vya kutoa maji vinafanyakazi kuwahudumia wakazi 235,000 huko Port-au-Prince. Inaeleza kua mpango wa chanjo kwa watoto umeanza, na wanatafuta maeneo salama kwa watoto kucheza. Hata hivyo idara hiyo inaeleza kwamba usalama wa watoto unabaki kua changamoto kuu.

Kwa upande wake Shirika la Afya Duniani WHO linasema mahitaji ya afya hivi sasa yanaingia katika awamu ya huduma baada ya matibabu. WHO inasema maelfu ya watu wamekatwa miguu au mikono baada ya kubanwa na vifusi na inasema kuna zaidi ya watu 120,000 wenye kuishi na HIV /Ukimwi huko Haiti wanaohitaji madawa yao ya ARV kwa haraka iwezekanavyo.

Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu UNFPA imesema kupunguza ghasia dhidi ya wanawake imekua kipau mbele chake kikuu, kwani kumekuwepo na ripoti za ubakaji na ghasia dhidi ya wanawake. UNFPA inasema katika hali ya fujo hatari za kutokea ghasia dhidi ya wanawake huongezeka.