Mkutano wa Kimataifa juu ya Haiti unafanyika Montreal

25 Januari 2010

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka sehemu mbali mbali za dunia, akiwemo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hilary Clinton, wanakutana Montreal, Canada Jumatatu asubuhi, kwa mkutano wa kimataifa juu ya namna ya kusaidia kukarabati taifa la Haiti lililoharibiwa na tetemeko la ardhi.

Mashirika manane ya kimataifa yanashiriki kwenye mkutano huo ambao waziri wa mambo ya nchi za nje wa Canada Lawrence Cannon aliueleza ni hatua muhimu ya kuikarabati Haiti. Waziri mkuu wa Haiti Jean-Max Bellerive anahudhuria pia mkutano huo.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Brazil Celso Luiz Amorim ameahidi kuongeza wanajeshi elfu moja mia tatu kusaidia kazi za Umoja wa Mataifa huko Haiti, alipoutembelea mji wa Port-au-Prine siku ya jumapili. Halikadhalika alisema sehemu ya msaada wa dola milioni 15 zilizotolewa na Brazil kwa msaada wa dharura inaweza kutumiwa katika miradi ya kuzalisha mapato kwa wa-Haiti inayongozwa hivi sasa na idara ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa UNDP ambayo tayari imeshawasaidia watu elfu 5.

Na wakati juhudi za dharura zinaendelea kwa kasi huko Haiti, zaidi ya wakazi wengine 235,000 (laki mbili elfu 35) wameuhama mji wakifaidika na usafiri wa bure unaotolewa na serekali kuuhama mji mkuu uloharibiwa kabisa na tetemeko la ardhi. Umoja wa mataifa umeleza Jumatatu kwamba inaminika kuna zaidi ya watu laki nane wanaoishi katika makambi ya kiholela katika sehemu mbali mbali za mji huo. Afisi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya huduma za dharura OCHA inasema hali ya wakazi kuuhama mji kwa wingi kuelekea maeneo ya mashambani na miji ya kaskazini na mashariki inatokana na matumaini kwamba huwenda maisha yakawa afadhali kidogo kuliko yalivyo katika mji mkuu kwa wakati huu, na mashirika ya huduma za dharura yanahangalika kutafuta hema kuwajengea wanaokimbia mji mkuu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter