Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCTAD: Uwekezaji wa Kigeni washuka sana mwaka 2009

UNCTAD: Uwekezaji wa Kigeni washuka sana mwaka 2009

Ripoti mpya ya Idara ya Biashara na maendeleo ya UM UNCTAD imegundua kwamba uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni FDI mwaka jana ulipungua katika kanda zote za dunia. Inaeleza kwamba mataifa yaliyoendelea yalishuhudia kuporomoka zaidi kwa uwekezaji mwaka 2008 na kuendelea kupunguka kwa mwaka 2009 kwa asili mia 41 zaidi.

Wataalam wa masuala ya uchumi wa UM wanasema hali kwa njia nyingi huwenda ikawa mbaya zaidi katika mataifa yanayoendelea. Mkurugenzi wa kitengo cha uwekezaji na ujasiri mali wa UNCTAD James Zhan anasema uwekezaji katika nchi hizi ulishuhudia viwango vya juu kabisa katika historia mapema mwaka 2008. Lakini anasema hali ilibadilika na kuanza kuporomoka hapo 2009 wakati athari za mzozo wa kifedha na kiuchumi duniani zilipoanza kujitokeza.

"Barani Afrika tumeshuhudia kupunguka kwa takriban asili mia 36 ya uwekezaji wa FDI. Na hii ni baada ya kufika kilele cha juu mwaka 2008 kwa Afrika. Na kupunguka kwa hali hii ni jambo la kutia wasi wasi kwa jumuia ya kimataifa na mashirika ya maendeleo kama sisi ambao tumeona uwekezaji jumla wa FDI ni takriban asili mia 29 ya fedha jumla zinazopatikana kwa bara la Afrika."

Zaidi ya hayo Zhan anasema uwekezaji wa kigeni kwa mataifa 33 maskini kabisa barani Afrika ulipunguka sana mwaka uliyopita kutokana na kudorora kwa mahitaji ya bidhaa kote duniani.

Ripoti imegundua hali ya muongezeko iliyokua ikiendelea kwa miaka sita huko Asia ikikoma kabisa. Inasema kanda hiyo ilishuhudia kuporomoka vibaya sana uwekezaji kwa mara ya kwanza tangu mzozo wa fedha wa Asia mwishoni mwa miaka 1990. Ripoti inaeleza kwamba kwa Amerika ya Kusini na Kati hali ilikua kadhalika mbaya ambako uwekezaji wa kigeni ulipungua kwa asili mia 41. Zhan anasema uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja hukabiliwa na hatari ya mabadiliko ya majira mbali mbali.

"Kama magari, kama bidhaa za fahari zinazohudsiana na uzalishaji zimepunguka sana. Na kuhusiana na bidha zisizokabiliwa na hatari kubwa kutokana na mabadiliko ya majira kama vile madawa, kilimo, mali asili hali imepunguka kidogo zaidi. Lakini haimanishi haikupunguka, lakini ni kwa kiwango kidogo zaidi. Na hiyo ni sawa kwa mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea."

Ripoti inaeleza kwamba mataifa sita yaliyopata uwekezaji mkubwa wa FDI 2009 ni Marekani, China, Ufaransa, Rashia, Uholanzi na Hong Kong.

UNCTAD imesema hali jumla ya uwekezaji wa kimataifa hata hivyo imeanza kuimarika. Matokeo yake, wataalam wanatarajia uwekezaji wa FDI utakua kwa wastani mwaka 2010. Waatalam wa uchumi wanasema hali inayoimarika hatimaye itayapatia motisha makampuni kuwekeza katika mataifa ya kigeni mwaka huu.