Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yasema watoto wako hatarini kusafirishwa nje ya Haiti kinyume cha sheria

UNICEF yasema watoto wako hatarini kusafirishwa nje ya Haiti kinyume cha sheria

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto UNICEF limeonya kwamba watoto walonusurika kutokana na tetemeko la ardhi huko Haiti wako hatarini kuchukuliwa kinyume cha sheria na watu wapotofu.

UNICEF inaeleza kwamba inabuni vituo vya muda vya kuwapokea watoto hasa wale ambao hawana watu wazima wanaofuatana nao ili waweze kua katika hali ya usalama.

Mshauri Mkuu wa Kikanda wa UNICEF kwa ajili ya ulinzi wa watoto Jean Claude Legrand anasema kwamba hata kabla ya maafa ya tetemeko la ardhi watoto huko Haiti walikua hatarani kutokana na biashara ya magendo: 

"Tumeshuhudia miaka iliyopita watoto wakichukuliwa nje ya nchi bila ya utaratibu wa kisheria. Jamii ya Haiti ina mundo thabiti na kuna jamaa za familia nyingi ambao wako tayari kuwachukua watoto na kua ni familia zao wenyewe. Kuna idadi kubwa ya wahaiti wanaoishi nchi za nje ambapo kuna familia wanaoishi Marekani, Canada na kwengineko ambao watakua tayari kuwaleya watoto hao kabla hata hawajapata vibali vinavyostahiki."

Legrand anasema kuna ushahidi ulopatikana unaonesha watoto wengi wamechukuliwa nje ya nchi kwa njia zisizo halali. Anasema wameorodhesha kiasi ya kesi 15 ya watoto kupotea kutoka hospitali bila ya familia zao kwa wakati huu.

Legrand anasema UNICEF na washirika wake wameunda mfumo wa ufuatiliaji, kuwaandikisha walotoweka na muhimu zaidi kujaribu kuzuia hali hiyo kutokea.