Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika yafanya maendeleo kuwafikia wathiriwa Haiti

Mashirika yafanya maendeleo kuwafikia wathiriwa Haiti

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaripoti kwamba wanafanya maendeleo makubwa katika kufikisha msaada wa dharura unaohitajika sana na maelfu ya walonusurika tetemeko la ardhi huko Haiti.

Afisi ya UM kuratibu huduma za dharura OCHA, inaeleza kwamba idadi ya tume wa kuokoa na kuwatafuta watu katika miji imefikia 52 kukiwepo wafanyakazi wa uwokozi elfu 1 820 na mbwa 175. Hadi hii leo kumekuwepo na watu ambao wameokolewa wakiwa hai chini ya vifusi, hata hivyo kungali na haja kubwa ya wahandisi na vifaa vikubwa vya kuondoa vifusi vikubwa kutokana na majengo yaliyoporomoka.

Idara ya chakula duniani WFP inasema hali katika maeneo yaliyoathirika vibaya inabadilika kila mara, kwani kunatokea mitetemeko midogo baada ya tetemeko kubwa na kuathiri juhudi za uwokozi. WFP inasema kumekuwepo na maendeleo katika kugawanya chakula, kwani hadi Jumatatu usiku takriban watu robo milioni walipokea chakula.

Idara ya watoto ya Umoja wa Mataifa UNICEF kwa upande wake inasema kipau mbele chao ni kuwalinda watoto na kuimarisha huduma za kuwapatia lishe bora. Inasema inafanya pia kila juhudi kuwaunganisha tena watoto na familia zao.

Idara ya Afya Duniani WHO inasema hivi sasa kuna Mashirika 20 ya afya wanaofanyakazi na wizara ya afya ya Haiti kwa kutoa huduma za dharura.