Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idara za UM kuimarisha juhudi za msaada kwa Haiti

Idara za UM kuimarisha juhudi za msaada kwa Haiti

Idara mbali mbali za umoja wa mataifa zimeanza kupanga mikakati ya muda mfupi kuisaidia Haiti na wananchi wake walokumbwa na maafa makubwa kutokana na tetemeko la ardhi mapema wiki hii.

Idara ya Chakula Duniani WFP inatayarisha mkakati wa miezi sita ya operesheni ya dharura kuwahudumia karibu watu milioni 2, kwa kuwapatia chakula kilichopikwa. WFP inasema tayari imeshapokea mchango wa zaidi ya dola milioni 20 kusaidia kazi zake huko Haiti.

Walinda amani wa UM wanaonya kwamba hasira zimeanza kuongezeka kutokana na hali kwamba msaada wa Haiti wanaotabika haitolewi kwa haraka. Msemaji wa kikosi cha Brazil huko Haiti David Wimburst anasema anahofu mambo yakabadilika na kila mtu anafahamu kwamba hali inavyozidi kua tete na watu maskini wenye haja kubwa wakiwa wanasubiri kuletewa chakula huenda wakazusha ghasia. Shirika la watoto UNICEF kwa upande wake inajaribu kuwatambua mayatima na kuwasaidia watoto wasojua mahala wazee wao waliko. Shirika la Afya WHO linasema kuzagaa kwa maiti kila mahali si kitisho kwa afya kwa wakati huu bali matatizo ya kiakili na kijamii. WHO haipendelei makaburi yanayozikwa watu wengi, na inatoa mwito wa kupatikana mikoba ya kutia maiti. Na msemaji wa WHO Paul Garwood anasema kiwango cha mahitaji ya huduma za afya ni kikubwa kisicho kua na mfano, na WHO inajaribu kuhakikisha mfumo usije ukaporomoka kabisa kwa kupeleka msaada kwa haraka.