Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aiomba jumuiya ya kimataifa kuisaidia Haiti

Ban aiomba jumuiya ya kimataifa kuisaidia Haiti

Katibu mkuu wa UM Ban Ki-moon ametoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuchangisha dola milioni 550 kuweza kukidhi mahitaji ya dharura ya wananchi wa Haiti walokumbwa na tetemeko la ardhi.

Takriban watu milioni 3 wameathiriwa na tetemeko la ardhi na Shirika la msalaba mwekundu linakisia kati ya watu elfu 45 hadi elfu 50 wamefariki na mahitaji muhimu hivi sasa ni kupata maji chakula na mahema kwa ajili ya walonusurika. Bw Ban alisema atakwenda Haiti wiki ijayo kushuhudia mwenyewe maafa yalitotokea.

"Makadirio ya awali kutoka kwa timu za dharura za umoja wa mataifa yanaonesha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu huko Port-au-Prince na maeneo mengine na karibu asili mia 50 ya majengo yaliyoharibika katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi."

Naibu katibu mkuu Bi Asha Rose Migiro anasema Umoja wa mataifa hivi sasa unalenga kuwasaidia wale walonusurika na tetemeko hilo kubwa huko Haiti.

Msemaji wa Bw Ban Martin Nesirky amesema hadi hivi sasa imethibitishwa kwamba watumishi 37 wa UM ndio wamefariki, wengine 330 bado hawajapatikana. 100 kati yao inaaminika wamenaswa chini ya kifusi cha Hoteli Christopher, iliyokua makao makuu ya Umoja wa Mataifa.