Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM unaihimiza Italia kupunguza chuki dhidi ya wageni

UM unaihimiza Italia kupunguza chuki dhidi ya wageni

Wataalamu wawili wa haki za binadamu wa UM wanaohusika na wahamiaji na ubaguzi wamewahimiza wakuu wa Italia kuchukua hatua zinazohitajika kupunguza hali ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya wafanyakazi wa kigeni.

Chuki hizo zilipelekea matukio ya kusikitisha wiki iliyopita katika mji wa Rosarno, kusini mwa Italia. Taarifa ya pamoja ya Mjumbe maalum wa UM kwa ajili ya haki za binadamu za wahamiaji, Jorge Bustamante na Mjumbe maalum wa UM kwa ajili ya ubaguzi mambo leo na chuki dhidi ya wageni Githui Muigai, inaeleza kwamba ghasia ikiwa imetendwa na wataliana au wafanyakazi wa kigeni ni lazima zikabiliwe kwa njia thabiti kupitia utawala wa sheria na ni lazima haki za binadamu zilindwe bila ya kujali hati ya mhamiaji. Karibu watu 53 walijeruhiwa mnamo siku mbili za ghasia na zaidi ya wahamiaji elfu moja walihamishwa vituo vya Bari na Crotone.