Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR: wananchi wathirika kutokana na kuzorota hali Somalia

UNHCR: wananchi wathirika kutokana na kuzorota hali Somalia

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), imeeleza kwamba kuongezeka kwa mapambano huko Somalia kunapelekea athari mbaya zaidi kwa wananchi na kusababisha idadi kubwa ya watu kukimbia makazi yao.

Zaidi ya watu 150 wanaripotiwa wameuwawa au kujeruhiwa na karibu elfu 7 wamepoteza makazi yao mnamo mapambano ya mwisho kati ya makundi yanayohasimiana ya wanaharakati. UNHCR inaeleza kwamba hali ya ukosefu wa usalama hairuhusu idara hiyo kuingilia kati mara moja, lakini inajadiliana na mashirika ya kiraia ya maeneo hayo kutafuta njia za kuwasilisha msaada wa dharura.

Andrej Mahecic, msemaji wa UNHCR huko Geneva anasema sehemu nyingi za Somalia ya Kati zinashuhudia ongezeko la mapigano, pamoja na sehemu za mji mkuu Mogadishu na Beled Weyne, mji mkuu wa wilaya ya Hiraan. Kutokana na mapigano, raia wa maeneo hayo wako hatarini, kwani huduma na uwezo wa kupata mahitaji muhimu imeharibika kabisa na kuzidi kupunguka. Anasema idadi ya wa-Somali wanaokimbilia mataifa jirani imeongezeka. Takriban wa-Somali elfu tatu wameandikishwa kama wakimbizi huko Ethiopia mwezi Disemba pekee. Huko Kenya zaidi ya wa-Somali elfu 4 wameandikishwa katika kambi ya Dadaab tangu mwezi wa Disemba.